KATIBU TFF AKATAA FEDHA ZA MATAJIRI WA SIMBA, YANGA

mwesigwa1 beb0f
KATIBU Mkuu mpya wa TFF, Selestine Mwesigwa ameingia ofisini na mkakati ambao hakuna tajiri yeyote wa Simba wala Yanga atataka kuusikia.
Kama mkakati huo utafanya kazi hakuna fedha zozote za mashabiki au wanachama matajiri zitatumika kufanya vurugu za usajili, jambo ambalo huenda likashitua wengi.
Yanga na Simba zimekuwa zikifanyiana vurugu kwa kupokonyana wachezaji wakati wa usajili huku wanachama matajiri ambao wengine si viongozi wakitaka kutunishiana ubabe na kuonyeshana nani mwenye fungu.
Lakini Mwesigwa ameingia TFF na mfumo ambao utazizuia klabu kutumia fedha yoyote ambayo haitokani na soka kama zilivyozowea kufanya Simba na Yanga ambazo hazina vyanzo maalum vya mapato.
Kwa mujibu wa Mwesigwa klabu zote za Ligi Kuu Bara zitatakiwa kujihadhari na matumizi ya fedha ambazo hazitokani na soka katika matumizi yake mbalimbali
ikiwemo usajili.

Mwesigwa aliliambia Mwanaspoti kwamba, moja ya mambo ambayo atayasimamia ni utekelezaji wa azimio la Bagamoyo ambalo lilielekeza mambo kadhaa ya kufuatwa ili kuendeleza soka nchini miongoni mwa mambo hayo ni klabu kuwa na watumishi wenye sifa, viwanja vya mazoezi na uwazi katika taarifa za mapato na matumizi.
Katika mapato na matumizi ndipo inapoingia hoja ya kuwepo kwa matumizi ya haki ya fedha za soka yaani 'Football Financial Fairplay', mfumo ambao unasimamiwa na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa).
"Football Financial Fairplay ndiyo itakayoongoza klabu kutumia fedha zinazotokana na soka tu na si vinginevyo, unajua hapa ndipo mambo yanapoharibika kwani unaweza kuona klabu moja inaidhamini klabu nyingine na kupunguza ushindani katika ligi," alisema Mwesigwa ambaye ni mtaalam wa uongozi wa biashara.
Mwesigwa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Yanga, alisema hata kama klabu zinasaidiwa na watu wenye fedha misaada hiyo inatakiwa kuwepo katika mikataba maalum na si mtu au kundi la watu binafsi kuingiza fedha kienyeji kwenye timu.
Klabu za Simba na Yanga mara nyingi zimekuwa zikifanya usajili wa wachezaji wake kwa kutumia mamilioni ya fedha ambazo hutoka kwa wapenzi na wanachama wake.
"Unajua hata Uefa baada ya kuona baadhi ya timu zinakuwa juu na nyingine zinaelekea kufa wakaanzisha hii 'Football Financial Fairplay' ili kuzipa nguvu na klabu nyingine, hivyo na mimi nitaisimamia ili kuona tunapiga hatua katika soka," alisema Mwesigwa mwenye umri wa miaka 43.
Hiyo inamaanisha kwamba kama klabu itataka kusajili itapaswa kutumia fedha zake yenyewe au ambazo zimetokana na udhamini ambao upo kwenye makubaliano maalum na si mwanachama au shabiki kutoa fungu ghafla. Chanzo: mwanaspoti

Comments

Popular posts from this blog