HAUSISIMKI UKIWA NAYE?

Wiki iliyopita tulikuwa na mada inayohusu jinsi tunavyoishi na familia zetu, nikauliza kama baadhi yetu huwa tunapata nafasi ya kujiuliza kuhusu vijana wetu, maana wengi huwa tunadhani baada ya kuwalipia ada, jukumu letu linaishia hapo.
Leo najaribu kuwa karibu na nyinyi katika upande mwingine. Na hii inatokana hasa na baadhi ya malalamiko ninayokutana nayo kutoka kwa wadau mbalimbali wa kona hii, wake kwa waume, wanaolalamikia jinsi wanavyojisikia wakati wa tendo la ndoa.
“Nashangaa sana, huwa sipati msisimko wowote ninapokutana na mpenzi wangu, sana sana huwa nasikia maumivu tu,” haya ni baadhi ya maneno ninayolalamikiwa na wadau wenzetu juu ya hisia zao.
Nimejaribu kubadilishana mawazo na watu kadhaa juu ya suala hili na wengi wamenieleza kuwa ni kweli hali kama hii hujitokeza, ingawa mara nyingi huwa ni kati ya mtu na mtu na wala siyo tatizo la kudumu la kila mmoja.
Kutosisimkwa kwaweza kutokea kwa sababu kadhaa, lakini kubwa ni kutovutiwa na mwenza wako. Waweza usinielewe, ninaposema kutovutiwa, namaanisha ninachosema. Wapo baadhi ya wenzetu huishi na wenza wao pasipo ridhiko la moyo.
Na hii inachangiwa na mambo mengi. Kuna mwanamke anaishi na mwanaume asiye chaguo lake la moyo kutokana na sababu za kiuchumi, hali ambayo pia inaweza kumkuta mwanaume.
Katika hali kama hii, mara nyingi ule msisimko wa kweli hauwezi kuwepo kwa sababu msisimko hutokana na hisia. Mtu anapokuwa na hisia kubwa za kimapenzi, ni rahisi nafsi yake kuridhika.
Hali kama hii unaweza kuishuhudia kwa mfano unapokutana na mtu ambaye kitendo cha kugusana tu na mwenzake, huweza kuharibikiwa. Huyu ni mtu ambaye hisia zake ziko juu na kwa maana hiyo, msisimko wake hauna mfano.
Lakini pia wapo ambao hukosa msisimko kutokana na matatizo ya kibaolojia, ingawa hawa ni wachache. Hawana hisia, hawasikii siyo tu raha, bali hata hamu ya tendo hilo hawana.
Mara nyingi inapotokea mtu akakosa msisimko, na hili hasa ni kwa wanawake, ni kwa sababu ya kutokuandaliwa vizuri. Baadhi ya watu hudhani maandalizi ni kupigana mabusu na kukumbatiana tu. Maandalizi mazuri zaidi ni pale unapojaribu kumshirikisha mwenzako tokea mwanzo.
Siyo vibaya kumuuliza mwenza wako ni jambo gani akifanyiwa atajisikia kusisimkwa. Badala ya kukimbilia ‘denda’, huenda mwenzio hujisikia zaidi akiguswa katika maeneo ambayo wewe labda hata huwezi kufikiria.
Hapa ndipo wengi wetu hukosea na kwa akina dada huzongwa zaidi na aibu. Wanadhani wakimwambia mwanaume kuwa wanapenda kufanyiwa hivi kabla ya tendo wataonekana malaya, kitu ambacho si kweli, kwani raha ya tendo ni kila mmoja alifurahie. Sasa kama hutaki kumweleza mwenzako inapopatikana furaha yako nani atakusaidia?
Kwa hiyo niwashauri wanaokosa msisimko kujaribu kuangalia kama wameshawahi kufanya baadhi ya mambo niliyozungumza hapa. Kama walijaribu mara kadhaa bila mafanikio, siyo jambo baya kutafuta mtaalamu wa saikolojia kwa sababu yaweza pia kuwa suala la kutokuwa sawa kisaikolojia.

Comments

Popular posts from this blog