John Mnyika ajitosa kuinusuru CHADEMA....Amejibu tuhuma moja tu ( ya kunga'ng'ania madaraka ) kati ya 6 zilizotolewa.

Mbunge wa jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CHADEMA, ndg John Mnyika amejitosa kukinusuru chama chake baada ya viongozi wakuu wa chama hicho kukabiliwa na tuhuma nzito zikiwemo za wizi wa fedha za wanachama na kung'ang'ania madaraka....

Yafuatayo ni majibu ya John Mnyika baada ya kutandikwa swali na mdau wa Mabadiliko kuhusiana na tuhuma ya kung'ang'ania madaraka kwa kubadili kinyemela baadhi ya vipengele vya katiba ya chama hicho.
KUMBU KUMBU MUHIMU:
(John Mnyika ni miongoni mwa wajumbe wa timu iliyofanya marekebisho ya Katiba mpya ya CHADEMA ya mwaka 2006.)

******Majibu yake ********

Ni kweli nilikuwa mjumbe kwenye timu zilizohusika na kuandikwa kwa katiba mpya ya CHADEMA ya mwaka 2006, aidha nilikuwepo kwenye mkutano mkuu wa chama uliopitisha katiba mpya tarehe 13 Agosti 2006.

Tuhuma ya kwanza toka kwa Mwigamba :
“Wakati tukifanya mabadiliko ya katiba mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitanomitano.
"Lakini wakati katiba inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela”.

Majibu ya John Mnyika:
Madai hayo hayana ukweli kwa kadiri ya ufahamu wangu.

Mosi, mwaka 2006 hatukufanya marekebisho ya katiba bali tuliandika upya katiba ya chama kutoka ile ya mwaka 2004. Waraka uliandikwa nchi nzima kwa wanachama kutoa maoni na kuwasilisha makao makuu kuanzia kwenye ngazi zao za chini za kikatiba.

Baada ya kukusanya maoni kulikuwa na timu tatu, timu moja ilihusu kuandika falsafa na itikadi ya chama ambayo Mwenyekiti wake alikuwa Profesa Baregu na katibu wake nilikuwa mimi.

Sehemu hiyo ya katiba niliandika neno kwa neno mapendekezo ya awali kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa, tulifanya mapitio pamoja na Profesa Baregu na hatimaye ikaingia kwenye vikao vya kikatiba vya chama na kupitishwa.

Sehemu ya falsafa kwa sehemu kubwa tulinukuu kwenye katiba kama ilivyokuwa mwaka 2004, sehemu ya itikadi tuliandika upya kabisa haikuwepo katika katiba ya CHADEMA ya zamani.

Sehemu zingine katika katiba kwa sehemu kubwa kazi ya kuunganisha maoni mapya na kufanya pia rejea kwenye katiba ya zamani ilifanywa na timu ya watu watatu tukiongozwa na muasisi wa chama Mzee Victor Kimesera pamoja na Mkurugenzi Benson Kigaila na mimi.

Kulikuwa na timu nyingine ya kuandaa miongozo ya mabaraza ya chama: Baraza la Wazee, BAVICHA na BAWACHA ambao nao walifanya kazi kwa upande wao na nilishiriki katika kupendekeza mwelekeo na mapitio ya kulinganisha rasimu ya miongozo yao na rasimu ya katiba ya chama.

Kwa ninavyokumbuka hicho kinachoitwa “kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano” hakijawahi kuingizwa kwenye katiba ya CHADEMA.

Baada ya timu zote kufanya kazi yake; rasimu ya katiba ilipita katika vikao vyote vya kikatiba yaani sekretariati, kamati kuu, baraza kuu na hatimaye mkutano mkuu. Katika vikao vyote hivyo, iwapo kipengele hicho kingekuwa kimeondolewa ‘kinyemela’ kama inavyodaiwa, mwandishi wa tuhuma hiyo angehoji toka Agosti 2006.

Aidha, baada ya katiba kupitishwa na kuanza kutumika kifungu hicho kingekuwa kimeondolewa kinyemela kati ya mwaka 2006 mpaka 2008 mtoa madai au mtu mwingine yeyote ndani ya chama angekuwa amehoji wakati wa matumizi. Kumekuwepo pia mchakato wa kufanya marejeo kwa ajili ya kushughulikia makosa ya uchapaji (errata) kwa nyakati mbalimbali, suala hili si kati ya mambo yaliyoibuliwa.

Mwaka 2009 CHADEMA kilifanya uchaguzi mkuu wakae mkuu nchi nzima ambapo vifungu vya masuala ya uchaguzi wa ndani ya chama vilifanyiwa rejea mara kwa mara. Mwandishi wa madai hayo alikuwepo wakati huo, suala hili la kwamba kuna kifungu kimeondolewa kinyemela sikulisikia likilalamikiwa kwenye vikao vyovyote vya kikatiba iwe ni sekretariati, kamati kuu, baraza kuu na mkutano mkuu.

Kwa vyovyote vile kwa historia ya chama toka mwaka kilipoanzishwa mpaka wakati huo wa uchaguzi wapo viongozi ambao walikuwa wanagombea wakiwa na vipindi viwili wakati huo kwenye cheo kimoja cha ngazi moja.

Kifungu hicho kingekuwepo toka 2006 kingetumika kuwawekea mapingamizi. Na kama kingekuwa ‘kimeondolewa kinyemela’ kungekuwa na malalamiko mengi kiko wapi kwa kuzingatia ‘joto’ la uchaguzi wa wakati huo.

2010 mpaka 2013 madai hayo hayajawahi kutolewa kwenye kikao chochote cha kikatiba katika ngazi ya taifa kwa kuwa mimi ni mjumbe wa vikao vyote vya kitaifa ambavyo yeye amesema kwamba ni mjumbe.

Madai kama hayo yangetolewa na asiye mwanachama au walau mwanachama wa kawaida tungesema tu ni maoni ya kawaida yaheshimiwe na aelimishwe. Lakini madai kama hayo yakitolewa na kiongozi wa chama mwenye nafasi ya kuujua ukweli wote huo yanaacha maswali kuhusu dhamira yake.

Naamini mamlaka zinazohusika za chama zitatumika katiba, kanuni, maadili na itifaki kuchunguza na kuchukua hatua kuanzia kwenye ngazi yao huko tukio lilipotokea.

Hata hivyo, kwa maoni binafsi (yasichukuliwe kuwa ni kauli ya nafasi ninazoshikilia kwenye chama), dhamira ya haya inajionyesha kwenye andiko lenyewe la muhusika kuanzia aya ya kwaza:( nimeinukuu hapo chini)
“ Kufuatia malumbano yanayoendelea kwenye vyombo vya habari na madhaifu mengi ambayo tumeshayashuhudia kwenye chama kwa sasa, natoa wito kwawana CHADEMA wote nchini kwamba wakati umefika tubadilishe uongozi wa juu wachama.

Mtoa madai anaendelea kuandika kwamba :( nimenukuu hapo chini )

“ Ni muhimu wanachadema mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania uenyekiti.
"Kama kingekuwepoleo Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba kugombea kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo kati yake na Zitto isingekuwepo na chama kingekuwa imara zaidi.
"Ni dhahiri Mbowe aliondoa kipengele hicho kwa makusudi ili aweze kuendelea kugombea bila mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa akina Lyatonga Mrema, John Cheyo na wengineo, na wanachadema hatupaswi kuuruhusu si kwa Mbowe tu balikwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama chetu."

Anaendelea kuandika madai mengine mengi lakini mwishoni anamalizia kwa dhamira yake ile ile :( nimenukuu hapo chini )
“ Nitaendelea kuwadondolea ili muonekwa nini napendekeza tuung'oe uongozi huu chini ya Mbowe.”.

Kwa hiyo, dhamira yake ni uchaguzi na mabadiliko ya uongozi; dhamira yeyote njema ifuate mkondo wa katiba, kanuni, maadili na itifaki; kinyume chake ni ‘njama ovu’ na ‘utovu wa maadili”.

Nimekuwepo chaguzi mbili kuu za CHADEMA 2004 (nikiwa mtazamaji sio mwanachama) na 2009 nikiwa katikati ya chaguzi hizo kama kiongozi.

Naamini uchaguzi huu wa chama ulioanza kuanzia mwaka huu 2013 utakamilika mwaka 2014 CHADEMA ikiendelea kusimamia dhima yake ya kuleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu.

John Mnyika

Comments

Popular posts from this blog