Diwani wa CHADEMA atiwa mbaroni kwa tuhuma za wizi wa milioni 10



WATU tisa akiwemo Diwani wa Kata ya Old Moshi Magharibi, Elisaria Mosha (Chadema) wametiwa mbaroni wakituhumiwa kupokea fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia mradi wa umeme mkoani Kilimanjaro.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal, kufanya ziara mkoani Kilimanjaro na kuagiza watu waliofanya hivyo wakamatwe mara moja.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema diwani huyo anatuhumiwa kujipatia Sh milioni 9.6 kwa njia ya udanganyifu.
Wengine wanaoshikiliwa ni Zakayo Kimathi (52) mkazi wa Mandaka, anayedaiwa kupokea Sh milioni 10.3, Oforo Kimambo (56) mkazi wa Mandaka anayedaiwa kupokea Sh milioni 29.
Wengine wanaotuhumiwa kupokea malipo hayo kwa njia ya udanganyifu ni Daud Mallya (69) mkazi wa Chekereni aliyepokea Sh milioni 8.6, Richard Mlaki (69) mkazi wa Kiboroloni alipokea Sh milioni 18.6 na Focus Herman (88) mkazi wa Kilototoni aliyepokea Sh milioni 36.
Boaz alisema kwa sasa watuhumiwa watatu hawajapatikana. Alieleza kuwa pamoja na watuhumiwa hao, polisi imemkamata Mwenyekiti wa Kijiji cha Mandaka Monono, Hassan Nduva (41) na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Vendelini Shayo (58) kwa kuhusika kufanikisha malipo hayo.
Dk Bilal alitoa agizo hilo mapema wiki hii wakati akizindua vituo vya kupozea na kusambaza umeme maeneo ya Kiyungi, YMCA na Makuyuni.
Alipokea taarifa kwa Mkuu wa Mkoa kuwapo kwa wananchi ambao hawakulipwa fidia zao, kutokana na kuwapo watu waliotumia ujanja wa kupokea fedha hizo, Sh milioni 169.2.
“Halmashauri ya Moshi Vijijini ndio ilikuwa wakala wa malipo hayo na ndio iliyofanya tathmini kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji, ambapo wao walipeleka tathmini hiyo kwa Shirika la Umeme (Tanesco), ambalo lilitoa fedha hizo hivyo Tanesco hawahusiki,” alisema,” alisema Boaz.

-Habari leo

Comments

Popular posts from this blog