Ofisi ya Pinda yatumika kutapeli

Mizengo-Pinda_d0c7b.jpg
MTANDAO wa watu wasiofahamika umetumia Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuandaa semina hewa kwa madiwani na wataalamu mbalimbali kutoka katika halmashauri za wilaya 16 nchini.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Bagamoyo juzi, baadhi ya madiwani na wataalamu waliotapeliwa walisema kuwa walipokea barua za mwaliko zikionyesha jina la ofisi hiyo zikiwataka wahudhurie semina ya siku nne kuhusu miradi ya maji katika miji midogo kuanzia Agosti 20-23, mwaka huu.
Barua hiyo yenye Kumb. Na PMO/RG/LG/TR/344 ya Agosti 12, mwaka huu, inaonyesha kusainiwa kwa niaba ya Katibu Mkuu Tamisemi na J. Sagini ikieleza kuwa ofisi hiyo kwa kushirikiana na nchi za Falme za Kiarabu iliandaa semina hiyo kwa ajili ya kutatua tatizo la maji.
Barua hiyo ilitumwa kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri za Biharamulo, Bunda, Bukombe, Maswa, Nkasi, Iramba, Karatu, Mufindi, Masasi, Muleba, Kibondo, Ngorongoro, Newala, Mbinga, Handeni na Ileje.
Wakurugrnzi hao walitakiwa kuwajulisha wajumbe wao ambao ni mwenyekiti wa halmashauri, madiwani watatu, mhandisi wa ujenzi, mhandisi wa maji na ofisa habari kuhudhuria semina hiyo katika chuo cha Mantep wilayani Bagamoyo.
"Sisi tulipata mwaliko wa barua kutoka Tamisemi Dodoma ambayo iko chini ya Waziri Mkuu tukitakiwa tufike hapa Mantep kwa ajili ya semina hiyo lakini tulichokikuta ni ukumbi uliokuwa umeandaliwa kwa ajili hiyo lakini wawezeshaji hawakuonekana," alisema, Ndila Mayeka, makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Maswa.
Viongozi hao walidai kuwa hiyo ni mara ya pili kwao kwani walishakwenda kuhudhuria semina kama hiyo mjini Bukoba Agosti 6, mwaka huu, lakini ikaahirishwa na mwaliko huo waliupata kupitia ofisi hiyo.
"Tulielezwa tutajulishwa na ndipo tukaitwa Bagamoyo lakini hatukukuta semina; huko ni kutumia vibaya fedha za walipa kodi," alisema Amina Almas, Diwani wa Kata ya Malampaka.
Naye Mkuu wa Chuo cha Mantep, Profesa Masanja, alisema kuwa walipokea mawasiliano ya barua pepe kutoka ofisi hiyo iliyotumwa na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Frola kwa niaba ya mhasibu mkuu wa Tamisemi ili waandae ukumbi kwa ajili ya semina hiyo lakini hawajawahi kumwona.
Akizungumzia kuhusu utapeli huo ambao umeleta usumbufu kwa wahusika, Mariamu Mbegu kwa niaba ya Katibu Mkuu Tamisemi alisema kuwa ofisi hiyo haijatoa mwaliko wa semina hiyo na kusisitiza kuwa barua hizo zimeghushiwa na hivyo kuahidi kumtafuta mtu au kikundi kinachotumia jina la ofisi ya Waziri Mkuu kwa mzaha.
"Hizi barua zilizotumwa kwa wakurugenzi wa halmashauri 16 ni feki kwani hata mwandiko uliotumika sio ambao tumekuwa tunautumia kwani ofisi yetu ina mwandiko wa aina moja katika barua zetu.
"Kwa tukio hili tutahakikisha tunampata mtu huyu au kikundi hiki ambacho kinaichafua ofisi ya Waziri Mkuu," alisema.
Mbegu aliwataka wakurugenzi wote wa halmashauri nchini kuwa makini wanapopata barua kutoka ngazi za juu iwapo wanaona zina mashaka ni vizuri kuwasiliana na mamlaka husika.
Hili ni tukio la pili kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusishwa na vitendo vya kughushi nyaraka kwani hivi karibuni mfanyabiashara, Amadi Popi (35), mkazi wa Dar es Salaam, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kughushi barua inayoonyesha imeandikwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Chanzo: Tanzania Daima

Comments

Popular posts from this blog