MFALME QABOOS ATOA MSAADA KWA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR



ZAZNa Kassim Ali na Amina Abeid (ZJMMC)
Sultan Qaboos wa Oman ametoa msaada wa Riali milioni tatu na laki moja za nchi hiyo  kwa ajili ya  ujenzi wa Msikiti mkubwa  utakaojengwa katika  eneo la Chuo cha Kiislamu Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
 Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mazizini,  Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamhuna amesema ujenzi  wa msikiti huo unatarajiwa kuanza  wakati wowote baada ya kutiwa saini makubaliano ya msingi kati ya Zanzibar na Oman.
Amesema msikiti huo, pamoja na shughuli za ibada, pia  utakuwa  ni chimbuko la kuanzishwa Chuo Kikuu cha Kiislamu Zanzibar na kufanikisha azma ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani karume aliependekeza kujengwa Chuo Kikuu cha Kiislamu katika eneo hilo alipokifungua chuo hicho.
“Maandaliz yote ya kujengwa msikiti huu yamekamilika na utakuwa na sehemu ya kusalia wanawake na wanaume, madarasa sita ya kusomea, chumba cha Kompyuta na  maktaba ya kisasa,” alieleza Waziri wa Elimu.

Akizungumzia msaada wa masomo ya Elimu ya juu uliotolewa na Mfalme Qaboos (Sultan Qaboos Academic Fellowship) kupitia Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) amesema umeanza kuleta mafanikio na wanafunzi wa kwanza 16 wataanza kufaidika na msaada huo mwaka huu.
Amesema wanafunzi tisa watasoma Digree ya tatu na saba watachukua Digree ya pili katika fani walizoomba na  watajiunga  kwenye  vyuo vikuu vya  nchi tofauti duniani.  
Ameongeza kuwa awali Wazanzibari 170 walipeleka maombi ya kupatiwa nafasi hizo kupitia mtandao na baada ya mchakato uliofanywa na kamati mbili zilizoundwa kushughulikia maombi hayo, waliobahatika ni watu 16.
Waziri Shamhuna amewatoa wasi wasi wananchi kuwa  hakukuwa na upendeleo wa aina yoyote katika kuwapata wanafunzi hao na kila kitu kilifanywa kwa njia ya mtandao.
“Tumekataa suala la ujomba au ushangazi katika nafasi hizi, tumetumia mtandao kuwapata wanafunzi bora na hao ndio waliofaulu kutokana na masomo waliyoomba na sifa walizanazo,”alisema Shamhuna.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali amesema hivi sasa wanaendelea kuboresha masomo ya sekondari na hivi Karibuni watakwenda Oman kuzungumzia  suala hilo ili kupata wanafunzi wengi zaidi wenye sifa za kujiunga kupitia msaada wa mfalme Qaboos.
“Elimu ya  ya juu haifikiwi mpaka wapatikane wanafunzi bora kutoka sekondari kwa hiyo ni lazima tujadili vipi tatawaboresha wanafunzi wa Sekondari,” alisema Waziri wa Elimu.
Amesema Oman na Zanzibar zimekuwa na mashirikiano makubwa katika nyanja mbali mbali ikiwemo Elimu na imefadhili Kongamano la Kimataifa litakalo zungumzia Ustaarabu wa Kiislamu katika nchi za Afrika Mashariki litakalofanyika kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 4 mwezi ujao Nungwi, Mkoa wa kaskazini Unguja.
Kongamano hilo limendaliwa na Taasisi ya Tafiti za Historia na Utamaduni ya Jumuia ya Nchi za Kiislamu Duniani kwa ushirikiano na Mamalaka ya kumbukumbu na nyaraka ya Falme ya Oman na wenyeji wa kongamano hilo ni Wizara ya Elimu Zanzibar ikishirikiana na SUZA.
Shamhuna ameongeza kuwa  Kongamano hilo litahudhuriwa na washiriki 170 kutoka Nchi 18 zikiwemo za Falme za Kiarabu, Mashariki ya mbali, Afrika Mashariki na Kati nchi za kusini mwa Afrika, Marekani na Ulaya.
Kongamano hilo litafunguliwa na  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohammmed Shein litafungwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKt Mohammed Gharib Bilal tarehe 4/9/2013.

Comments

Popular posts from this blog