MCL sasa kuwajaza wasomaji mamilioni, magari matatu;

chomoka_02624.jpg
Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), imezindua promosheni kabambe ya 'Chomoka na Mwananchi' itakayowawezesha wasomaji wa gazeti la Mwananchi, kujishindia zawadi zenye thamani ya Sh250,000,000.Zawadi hizo ni pamoja na fedha taslimu na magari matatu mapya.
Akizungumza katika uzinduzi huo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Tido Mhando, alisema promosheni hiyo itakayoanza leo, itafanyika nchini kote kwa siku 100 na kila siku kutakuwa na mshindi ambaye atajinyakulia Sh1,000,000.
P.T

"Hii ni promosheni ambayo lengo lake ni kuwashukuru wasomaji wetu kwa kuendelea kulipenda gazeti lao na kuliweka juu hapa nchini," alisema Mhando.
Alisema hadi mwisho wa promosheni hiyo (Novemba 30, mwaka huu), wasomaji 100 watakuwa wamejinyakulia fedha taslimu Sh100,000,000 na wengine watatu watapata magari mapya.
"Lengo letu ni kuwawezesha wasomaji siyo tu kupata habari na kufikiri tofauti, bali pia kuweza kuwajenga kimaisha," alisema Mhando.
Alisema promosheni hiyo itaendeshwa na MCL kwa kushirikiana na Kampuni ya Push Mobile.
Alitaja magari ambayo yatanyakuliwa na wasomaji kuwa ni Vista, Manza na Tata Safari.
"Haya ni magari mapya kabisa kutoka kiwandani," alisema.
Jinsi ya kushiriki
Alisema kuwa ili kushiriki promosheni hiyo, msomaji wa gazeti la Mwananchi, atatakiwa kujipatia nakala ya siku husika na atakuta namba maalumu ya ushiriki ikiwa imebandikwa kwenye jarida lililomo ndani ya gazeti hilo.
"Kila nakala ya kila gazeti kwa kila siku itakuwa na namba maalumu ya ushiriki inayojitegemea kabisa bila kufanana na namba nyingine, msomaji atatakiwa kutuma namba hiyo ya ushiriki kwa ujumbe mfupi wa simu (sms) kwenda namba 15584 na hapo atakuwa ameingia kwenye droo ya Sh1,000,000 ya siku husika na droo ya magari matatu," alisema. Mkurugenzi huyo alisema ujumbe huo utatozwa Sh200.

Comments

Popular posts from this blog