MASHEIKH DAR WAMKINGIA KIFUAA LOWASSA



TAASISI ya Amani ya Kiislamu (TIPF), imewapongeza viongozi mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kutokana na michango yao ya maendeleo katika jamii. Taasisi hiyo imempongeza Lowassa kutokana na jitihada zake za kuendesha harambee iliyowezesha kukusanywa Sh milioni 520, kwa ajili yakuchangia redio ya kiislamu ya Mkoa wa Mwanza, IQRA FM. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Sheikh Sadiki Godigodi, alisema viongozi wa aina hiyo ni mfano wa kuigwa na kupigiwa mfano.

“Tunampongeza kwa kuwa ni jambo kubwa sana na zito alilolifanya kwa maendeleo ya dini yetu, kwani redio hiyo itasaidia kutoa elimu ya dini na hofu ya Mungu katika jamii.

“Viongozi wa aina hii wasiokuwa na ubaguzi wa dini katika kuchangia maendeleo ni mfano mzuri, hatuwezi kuwavunja moyo kwa kuwabeza, jamii inapaswa kutambua mchango wao. 
Mwingine hapa ni Mwenyekiti mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, ni miongoni mwa watu waliopewa tuzo ya kutambua mchango wake katika jamii,” alisema.
Sheikh Godigodi alimtaka Lowassa kupuuza kauli hasi zinazotolewa na baadhi ya masheikh na waumini wa dini ya kiislamu kuhusu hatua yake ya kuchangisha fedha misikitini na makanisani.
“Haya ni maneno yasiyokuwa na msingi wala tija yoyote, Lowassa hakuangalia imani yake, alikwenda pale Mwanza kaendesha harambee kubwa na fedha imepatikana ya kutosha.
“Radio Quran ya jijini Dar es Salaam wanamahitaji ya fedha, waliitisha harambee na kufanya michango mbalimbali, lakini katika Sh milioni 80 walizokuwa wanahitaji, walipata Sh milioni 21 tu.
“Imekuwaje wamepata kiasi kidogo kama hicho wakati Waislamu wapo, masheikh wapo tena karibu robo tatu ya wafanyabiashara wa Dar es Salaam ni Waislamu, hivi ni kweli wameshindwa kuikwamua Radio Quran kwa kutoa milioni 80?
“Leo hii Lowassa pamoja na kwamba ni Mkristo, hakujali imani yake amechangisha milioni 520 yeye mwenyewe katoa milioni 20 kwa ajili ya redio ya kiislamu na Waislamu wapo wametoa macho tu.
“Sasa mtu wa namna hii unambeza vipi? Kama kiongozi amefanya jambo jema katika jamii, anastahili kupongezwa na si kubezwa kama wanavyosema hao watu wengine.
“Hata kama kuna mambo yalifanyika huko nyuma, lakini Lowassa bado ni kiongozi, Mbunge wa Monduli, ni Mwenyekiti wa kamati ya Bunge, pia aliwahi kuwa waziri mkuu, kwa hiyo bado anastahili kuheshimiwa,” alisema.
Sheikh Godigodi ambaye aliongozana na Sheikh Othman Mohamed, aliitahadharisha jamii kuepuka kauli zenye kuashiria ubaguzi wa kidini na badala yake wajenge umoja na mshikamano.
Sheikh Godigodi pia alitumia jukwaa hilo kumsifu Rais Jakaya Kikwete, akisema kuwa safari zake za nje ya nchi zimesaidia kuitangaza Tanzania katika medani ya kimataifa.
“Tunampongeza Rais Kikwete kwa juhudi zake za kuitangaza nchi yetu kimataifa na kuiletea maendeleo makubwa yanayotokana na ziara zake za nje ya nchi, ingawa baadhi ya watu wamekuwa wakibeza.
“Watanzania hatuhitaji kuambiwa, sisi wenyewe tunaona matunda ya ziara zake, tumeshuhudia ujio wa Rais wa Marekani na Rais wa China, zote hizi ni jitihada zake.
“Kama ilivyo anuani ya taasisi yetu kuwa ni ya amani, tunawaomba Watanzania tudumishe amani katika nchi yetu kwani pasipo na amani hakuna maendeleo,” alisema.


MTANZANIA

Comments

Popular posts from this blog