JWTZ KUONGEZA NGUVU ZAIDI DARFUR BAADA YA VIFO VYA ASKARI WAKE SABA...


 
Mkurugenzi wa Habari na uhusiano wa Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe alipokuwa akizungumzia kuuawa kwa askari 7 wa Tanzania na wengine 14 kujeruhiwa na waasi Darfur Sudan juzi.Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), linatarajia kuongeza nguvu ya kujilinda, wakati wa kulinda amani katika Jimbo la Darfur nchini Sudan, ili kujikinga na mashambulizi kama la juzi, ambalo lilisababisha askari wake saba kupoteza maisha.

Msemaji wa JWTZ Kanali Kapambala Mgawe, alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumzia shambulio hilo, lililosababisha pia majeruhi wengine 14.

Kanali Mgawe alisema mawasiliano yanafanyika kati JWTZ na Umoja wa Mataifa (UN), kuhusu uwezekano wa kuongeza uwezo wa kujilinda na mashambulizi, wakati askari wa Tanzania  wanapokabiliana na mashambulizi hayo.

"Kama inavyojulikana, kikosi chetu kipo kule kulinda amani kwa mujibu wa makubaliano ya Umoja wa Mataifa (UN) Sura ya Sita, ambayo yanataka kusitumike nguvu sana, sasa tunataka tutumie Sura ya Saba inayotoa fursa ya kuongeza uwezo wa kujilinda. 
"Mawasiliano yanafanyika kati yetu na UN kuhusu uwezekano wa kuongeza uwezo wa kujilinda na mashambulizi wakati wa mashambulizi hayo," alisema Kanali Mgawe.
Kanali Mgawe alisema wanajeshi hao wanaounda kikosi cha wanajeshi 875, walikuwa sehemu ya askari 37 na ofisa mmoja.
Walipatwa na mkasa huo saa tatu asubuhi juzi Jumamosi, wakati wakisindikiza msafara wa waangalizi wa amani kutoka eneo la Khor Abeche kwenda Nyara, Darfur na ghafla walishambuliwa na kikundi cha waasi wa Sudan.
Kanali Mgawe alisema kutokana na majukumu ya  kikosi hicho  na  makubaliano ya  UN Sura ya Sita, haikuwa rahisi kufikiria kuwa wangekutana na shambulizi hilo, kwa kuwa hata eneo hilo halina historia ya matukio kama hayo.
Taarifa ya Msemaji wa Vikosi vya UN, Chris Cycmanick iliyotolewa juzi jioni, ilieleza kuwa shambulio hilo lilifanywa na kundi kubwa la watu waliokuwa na silaha nzito za kivita, ikiwemo mabomu ya kutupwa kwa roketi.
Cycmanick alisema shambulio hilo, lilitokea kilometa 20 kutoka  makao makuu ya kikosi hicho, Khor Abeche na Kikosi cha Uokoaji kilifika baadaye kunusuru majeruhi 14, akiwemo askari Polisi mmoja.
Miili ya marehemu hao na majeruhi, waliondolewa na kupelekwa Nyara kwenye Hospitali Kuu ya eneo la Operesheni, kuhifadhi  miili  na kutoa matibabu kwa majeruhi.
JWTZ kwa sasa inawasiliana na familia za marehemu, kuhusu taratibu za mazishi na UN kwa ajili ya taratibu za matibabu kwa askari wote, waliojeruhiwa katika eneo la tukio.
Kanali Mgawe aliahidi JWTZ itaendelea kutoa taarifa kuhusu tukio hilo kadri watakavyozipata, baada ya ujumbe wa Tanzania uliotumwa Darfur kuwasili nchini.

Comments

Popular posts from this blog