DHAMBI KUBWA YA WANAWAKE WANAOJIFANANISHA KIUME NA WANAUME WANAOJIFANANISHA KIKE.



Mwenyezi Mungu S.W.T. amewalani wanawake wanaojifananisha kiume na wanaume wanaojifananisha kike, na ndio maana ikawa ni katika madhambi makubwa sabini. Mfano wa kujifananisha ni kama vile: Kuzungumza, kutembea, kuvaa mavazi; na kwa wanawake, kumpenda mwanamke mwingine kama wanaume kwa ajili ya kusagana wanawake kwa wanawake (Lesbians), na kwa wanaume, ni kuingiliana wanaume kwa wanaume (Homosexuals). Kutokana na maumbile ya Mwenyezi Mungu S.W.T. ameumba wanaume na ameumba wanawake, na tabia zao na mavazi yao na msemo wao ni tofauti kabisa, lakini ikiwa mwanamume atajifananisha kuwa sawa na mwanamke au mwanamke kuwa sawa na mwanamume, basi watakuwa wamezibadili wao wenyewe taratibu walizopangiwa na kuwekewa na Mola wao, na kwahivyo watakuwa wametenda dhambi kubwa. Mtume S.A.W. kasema katika Hadithi iliyotolewa na L-Bukhari, “

‘‘لَعَنَ الله الْمُتَشَبِّهَاتِ مِنَ النِّسَاءِ بِالرِّجَالِ وَالْمُتَشَبِّهِينَ مِنَ الرِّجَالِ بِالنِّسَاءِ’’
Maana yake, “Wamelaaniwa na Mwenyezi Mungu wanaojifananisha wanawake kiume na wanaojifananisha wanaume kike.” 
Pia Mtume S.A.W. kasema katika Hadithi nyingine iliyopokelewa na Ibn Abbaas R.A.A. na kutolewa na Abu Daud, “
‘‘لَعَنَ اللَّه الْمُخَنَّثِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالْمُتَرَجِّلاتِ مِنَ النِّسَاءِ’’
Maana yake, “Mwenyezi Mungu amewalani wanaume wanaojifananisha kike na wanawake wanaojifananisha kiume.” 
Na pia Mtume S.A.W. kasema Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na kutolewa na L-Bukhari, “
‘‘لَعَنَ اللَّه المرأة تلبس لبسة الرِّجَالِ والرِّجَالِ يلبس لبسة المرأة’’
Maana yake, “Mwenyezi Mungu amemlani mwanamke anaevaa mavazi ya kiume na mwanamume anaevaa mavazi ya kike.” 
Na ikiwa mwanamke kaolewa, na mumewe yuko radhi na kitendo hiki na hataki kumzuia kwa tabia hii, huwa naye pia anashiriki kwa sababu ya kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Tahriim aya ya 6, “يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ... 
Maana yake, “Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu, na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe...”
Mwanaume anabeba masuulia makubwa ya kumfundisha dini mkewe na wanae ili wamtii Mwenyezi Mungu S.W.T. na kuwazuia kufanya maasi. Na asipofanya hivyo ataulizwa kesho siku ya Kiyama na atashindwa kujibu. Na pia mke anabeba masuulia ya ulinzi wa nyumba ya mumewe na watoto wake. Mtume S.A.W. kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn `Umar R.A.A. na kutolewa na L-Bukhari na Muslim, “
‘‘كُلُّكُمْ رَاعٍ وَكُلُّكُمْ مَسْئُولٌ عن رعيته . الرَّجُلُ رَاعٍ في أَهْلِهِ وَمَسْئُولٌ عنهم يوم القيامة’’
Maana yake, “Nyinyi nyote ni walinzi na nyinyi nyote mtaulizwa (kila mmoja wenu) kwa ulinzi wake. Mwanamume ni mlinzi kwa watu wake (mkewe na wanawe) na ataulizwa juu yao siku ya Kiyama.”
Mtume S.A.W. kasema: Kuwatii wanawake kwa maasi ni kuangamizwa kwa wanaume, katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na kutolewa na Muslim, “
‘‘ألآ هَلَكَتْ الرِّجَالُ حين أطَاعُوا النِّسَاء’’
Maana yake, “Kwa kweli, wanaume wanaangamia wakati wanapowatii wanawake (kwa maasi).” 
Na pia Uislamu umewaharamishia wanawake kuvaa nguo ambazo hazifuniki miili yao vizuri. Na kuvaa zile nguo za kubana zinazoonesha maumbile ya maungo yao na hasa zile sehemu zinazowavutia wanaume ndizo zenye kuleta fitina kubwa. Mtume S.A.W. kafananisha uchanaji wa nywele zao wanawake hao kama nundu ya ngamia. Na huu ni muujiza mkubwa wa Mtume S.A.W. kwani kama vile aliwaona wanawake wa sasa mavazi yao na uchanaji wao, ambapo zama zake hapakuwepo na wanawake wa aina hii. Mtume S.A.W. kaongezea kusema: Wanawake wa aina hii hawatoingia Peponi, katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na kutolewa na Muslim, “
‘‘نِسَاءٌ كَاسِيَاتٌ عَارِيَاتٌ مُمِيلاتٌ مَائِلاتٌ ، رُءُوسُهُنَّ كَأَسْنِمَةِ الْبُخْتِ الْمَائِلَةِ ، لا يَدْخُلْنَ الْجَنَّةَ وَلا يَجِدْنَ رِيحَهَا وَإِنَّ رِيحَهَا لَيُوجَدُ مِنْ مَسِيرَةِ كَذَا وَكَذَا’’
Maana yake, “Wanawake wamevaa mavazi ya uchi (yaani ingawa wamevaa nguo lakini wako uchi, kwa sababu ya nguo zao nyepesi zinaonesha miili yao, na nguo za kubana zinazoonesha umbile la maungo yao) wameelemea kuinama (kwa kupenda kuvaa nguo za kutojisitiri), (kwa namna walivyochana nywele zao) vichwa vyao (vimefanana) kama nundu za ngamia vimeinama, hawataingia Peponi wala hawatapata harufu yake. Na hakika harufu yake inapatikana kutoka umbali wa hivi na hivi.”

Comments

Popular posts from this blog